About Me

Morogoro, Morogoro mjini, Tanzania

Monday 2 January 2017

KILIMO BORA CHA CHOROKO

UTANGULIZI


Choroko ni zao la chakula na biashara lenye kiasi kikubwa cha protini na madini ya phosphorus na calicium.Zao hili likilimwa vizuri hutoa mavuno kati ya Kg 400 hadi 900 kwa ekari.
UDONGO NA HALI YA HEWA IFAAYO.

Choroko hustawi katika udongo wa aina tofauti tofauti usiotuamisha maji.Hulimwa kutoka mita 0 hadi 1500 kutoka usawa wa bahari japokuwa kuna mbegu nyingine zinaweza kukubali zaidi ya ukanda huu.Hili ni zao linalostahimili ukame.
AINA ZA CHOROKO

Kuna aina kuu mbili za choroko ambazo pia zimegawanyika katika makundi mawili,choroko nyeusi na choroko za kijani.
1>CHOROKO ZINAZOTAMBAA-hizi ni choroko ambazo zinarefuka sana na hutambaa sehemu mbalimbali.

2>CHOROKO ZINAZOSIMAA=Hizi ni choroko ambazo zinakuwa kwa kusima kwenda juu.Hizi huchukua muda mfupi kukomaa wastani wa siku 60-70


Image result for picture of mung bean plantKIPINDI KIZURI CHA UPANDAJI WA CHOROKO

Choroko hazihitaji maji mengi hivyo ni budi zipandwe mwishoni mwa msimu wa mvua,Pia zinaweza kupandwa katika shamba lililolimwa mpunga.


NAFASI ZA UPANDAJI WA CHOROKO NA KIASI CHA MBEGU

Choroko huitaji mbegu kiasi cha kilogram 8 hadi kumi kwa ekari moja.
Panda choroko zako kwa nafasi ya sentimeta 30 mastari na mstari na sentimeta 10 shina hadi shina (30 x10 )sentimeta au (40 x 8 )sentimeta


SAMADI NA MBOLEA ZA VIWANDANI

Kama shmba lako halina rutuba ya kutosha unaweza kuongeza samadi kiasi cha tani tano kwa ekari na pia unaweza kupanda kwa kutumia mbolea ya NPK kg 50 kwa ekari.weka mbolea zote kabla ya kupanda.


UMWAGILIAJI

Kama umepanda kipindi cha ukame sana au unalima kilimo cha umwagiliaji basi mwagilia shamba lako upate unyevu wa kuotesha mbegu, kisha baada ya mbegu kuota kaa siku 6 hadi 10 na umawgilie tena. Mara tatu za kumwagilia zinatosha kwa choroko.
PALIZI

Palilia shamba lako mapema kuzuia magugu.Palizi moja inaweza kutosha.


MAGONJWA YA CHOROKO

1-yellow mosaic virus ( Ugonjwa wa manjano)
Dalili- mmea unakuwa wa njano na madoa ya njano katika majani.
Kinga na tiba-Panda mbegu zinazostahimili magonjwa.


2-Powdery Mildew (Ukungu)

Dalili-Majani yanakuwa na vidoti vya njano ambavyo vinabadilika kuwa vya kahawia au kijivu haraka na ambapo kunakuwa na unga unga katika majani.
Kinga na tiba-Panda mbegu zinazostahimili ukungu,Pulizia dawa za ukungu (Fungicide).
anza kupuliza wiki tatu baada ya mimea kuota na kuendelea kulingana na hali halisi.


3> LEAF SPOT (Vidoti katika majani)

Dalili-majani yanakuwa na vidoti vya mviringo na visivyo na umbo maalum ambapo katikati yanakuwa na rangi rangi ya kijivu na weupe na mistari ya rangi ya wekundu-kahawia au nyeusi-kahawia.ugonjwa huu husababisha hasara hadi ya asilimia 58 ya mapato.
Kinga na Tiba-Panda mbegu inayostahimili ugonjwa huu,Choma mabaki ya mimea hii na ile ya jamii moja baada ya kuvuna.Pulizia dawa za ukungu (Fungicide) Katika nafasi ya wiki mbili mbili kama eneo hilom linashambuliwa mara kwa mara na ukungu


WADUDU.

Kuna wadudu mbalimbali wanaoshambulia choroko kama vile aphidi,funza wa vitumba,nzi wa maharage.Wazui wadudu hawa kwa kupuliza dawa za wadudu mara tu baada ya mimea kuota,dawa kama karate,twigathoate,dimethote na nyinginezo zinaweza kutumika.


UVUNAJI

Mara tuu choroko zinapofikia asilimia 85 ya ukaukaji zinabidi zivunwe ukichelewa zitapukutikia shambani...Kwa Ushaur zaidi piga simu namba 0718405318 kutana idara makini ya washauri hapa (KMT )Kilimo na mkulima Tanzania


Tuesday 27 December 2016


http://ichef-1.bbci.co.uk/news/ws/640/amz/worldservice/live/assets/images/2015/09/16/150916094624_cassava_640x360_spl.jpgKILIMO CHA MUHOGO
Zao la muhogo ni muhimu sana kwa Tanzania zaidi kwa wakulima wadogo wenye kipato cha chini. Wakulima wengi huchanganya zao la muhogo na mazao mengine kama vile kunde, mbaazi, njugumawe, n.k. Umuhimu wa zao hili ni kutupatia cahakula na wakati mwingine kwa biashara. Kwa kanda ya kusini muhogo ni chakula kikuu ambacho kinachukua asilimia 75 ya chakula kwa maeneo yote ya mikoa ya pwani

Muhogo hustawi vizuri katika maeneo yaliyopo kwenye maeneo ya mita 0 – 1500 kutoka usawa wa bahari. Vile vile muhogo hustawi vizuri kwenye maeneo yanayopata mvua ya wastani wa mm 750 - mm1200 kwa mwaka. Muhogo hustawi vizuri kwenye ardhi ya kichanga. Vili vile zao la muhogo ni maarufu sana kwa uvumilivu wa hali ya ukame.

TEKNOLOJIA ZILIZOPO
Mbegu bora za muhogo
Mpaka sasa hivi kuna aina mbili za mbegu bora ambazo zimathibitishwa kwa wakulima. Mbegu hizi huvumilia magonjwa, (batobato na matekenya), pia huzaa sana ukilinganisha na mbegu za kienyeji.

Naliendele
Huzaa tani 19 kwa hekta moja, na inaweza kuvunwa kuanzia miezi 9 toka ipandwe.

Kiroba
Huzaa tani 25 – 30 kwa hekta moja, na inaweza kuvunwa kuanzia miezi 9 toka ipandwe.

Mbinu bora za kilimo cha muhogo

Uandaaji wa shamba
Shamba liandaliwe kabla ya msimu wa kuanza. Uandaaji wa shamba bora hufuata hatua zifuatazo:
- Kufyeka shamba
- Kung’oa na kuchoma visiki
- Kulima na kutengeneza matuta

Uchaguzi wa mbegu bora za kupanda
Mbegu zinatakiwa zisiwe na magojwa yeyote, pia chagua mashina ambayo yamekomaa vizuri.

Upandaji
Kuna njia tatu za upandaji wa muhogo:
- Kulaza ardhini (Horizontal)
- Kusimamisha wima (Vertcal)
- Kuinamisha ( Inclined/Slunted)

Urefu wa kipande cha shina cha kupanda:
Inashauriwa urefu uwe sm 30; lakini urefu wa kipande cha kupanda unategemea sana idadi ya macho yaliyopo kwenye hicho kipande, inashauriwa kipande kiwe na macho (4 – 6).

Nafasi ya kupanda:
Kwa upandaji wa shamba muhogo tupu, shina hadi shina ni mita 1 na mstari hadi mstari ni mita 1.Kwa shamba la mchanganyiko na mazao mengine, inategemeana na zao linalochanganywa; mstari hadi mstari ni mita 2 – mita 4 na shina hadi shina ni mita 1.


Palizi:
- Palizi ya kwanza ifanyike mapema (mwezi 1) baada ya kupanda ili kuepukana na magugu yanayochipua haraka baada ya mvua kunyesha. Ndani ya miezi mine ya mwanzo mihogo haitakiwi kuwa na magugu ili kuepuka ushindni wa mahitaji muhimu (mwanga, mbolea, maji, n.k) kati ya muhugo na magugu.
- Palizi hufanyika kwa kutumi jebe la mkono au dawa ya kuuwa magugu.
- Wakati mwingine udhibiti wa magugu kufanyika kwa kutumia majani kwa kutandazwa juu ya udongo.
- Plaizi hufanyika mara 2 – 3 hadi muhugo kukomaa.

Uvunaji:
Mihogo inaweza kuanza kuvunwa baada ya miezi 9 – 12 tangu kupandwa. Inashauriwa kuvuna katika katika kipindi cha jua; kwani wakati wa mvua kiwango cha wanga kwenye muhogo hupungua.

Usindikaji bora
Usindikaji bora wa muhogo unafanyika kwa sababu kuu mbili:
- Kurahisisha/kuharakisha ukaushaji
- Kuondoa sumu (cyanide) ilyoko kwenye baadhi ya aina za mihogo
- Kuongeza ubora wa unga utokanao muhogo wenyewe.

Njia bora za usindikaji
- Kwa kutumia mashine aina ya Grater
Hii hutoa chembechembe laini za muhogo, ambazo baadae hukamuliwa kwa kutumia kifaa kingine kiitwacho “presser” ili kuondo sumu iliyoko kwenye muhogo. Mashine hii hutumika hususani kwa muhogo mchungu.
- Kwa kutumia mashine aina ya chipper
- Mashine hii hutoa vipande vidogo vidogo (chips). Mashine hii hutumika hasa hasa kwa ajili ya mihogo mitamu/baridi.

Matumizi ya Muhogo
- Muhogo unaweza kupikwa wenyewe kama chakula au kutengeneza unga
- Unga wa muhogo unaweza kutengeneza vitu vyotekama vinavyotengenezwa na unga wa ngano kama vile biskuti, chapatti, maandazi, chichili, keki n.k.
- Pia muhogo huweza kutumika viwandani kutengeneza bidhaa nyingine kama vile wanga.


MAGONJWA NA WADUDU WAHARIBIFU
Magonjwa
Kuna magonjwa mawili ambayo ni muhimu sana na yanapunguza uzalishaji wa zao la muhogo.

a) Ugonjwa wa Matekenya au Ugonjwa wa michirizi ya kahawia
katika muhogo
Ugonjwa huu ni maarufu kwenye sehemu zenye miinuko iliyo na urefu chini ya mita 300 na unapatikana kidogo sana kwenye miinuko ya mita 500 na kuendelea ambako uenezaji wake wa kawaida hautokei kabisa.

Visababishi:
Matokeo ya uchunguzi wa awali unaonyesha kwamba ugonjwa huu ulienezwa na mdudu mweuupe au inzi mweupe (whitefly) mwenye mabawa madogo.

Dalili za Ugonjwa
Sehemui zote za muhogo zinaweza kuonyesha dalili za uambukizo wa ugonjwa huu lakini ni vipengele gani vya ugonjwa na ni kwa kiwango gani hutegemea hali ya mzingira, hatua ya kukua kwa mmea kwa kulinganisha.

- Kwenye majani
Dalili ya kwanza: Chlorosis rangi ya njani hutokea kwanza pembezoni mwa vena ndogo baadae huathtiri vena ndogo zaidi na inaweza kuwa doa (chlorosis) la rangi ya njano.
Dalili ya pili: Rangi ya njano ambayo haihusishwi vizuri na vena isipokuwa katika mbaka ya mviringo kati ya vena kuu kwenye hatua za mwisho za ugonjwa sehemu kubwa ya lamin inaweza isiathirike, majni yenye ugonjwa hubaki yameshikilia kwenye mmea kwa muda wa wiki kadhaa.

- Kwenye shina
Huonekana kwenye tisu ya shina changa la kijani, jeraha la zambarau au kahawia linweza kuoneakan nje na kuingia ndani hadi kwenye gamba baaada ya kubandua gome la nje. Pia jeraha la nekrotiki kwenye kovu la shina hutokea baada ya majni kudondoka kutokana na umri wa mmea. Tawi/shina hufa kuanzia kwenye nch kuelekea chini na kusababisha kufa kwa mmea wote.

- Kwenye mizizi
Kwa kawaida hutokea baada ya dalili za majani na wakati wa kipindi kati ya uambukizo na kufa, amabpo kifo cha mizizi hutokea kuanzia miezi 5 toka kupandwa. Dalili za mizizi zinabadilika nje ya mizizi na zinaweza kuwa kama kizuizimwanga au shimo au kufa kwenye gome.

Tishu inayo zunguka mshins ina doa la rangi ya kahawia au nyeusi. Wakati mwingine mizizi huonekana kuwa yenye afya kwa nje bila kuwa na matatizo yaliyowazi au bila kupungua ukubwa, lakini ikikatwa huonekana kufainakufa au rangi ya njano.

Uambukizaji na ueneaji
Ugonjwa wa CBSD unaambukizwa kwa njia ya vipandikizi vinavyotokea kwenye mimea iliyoathiriwa vinavyosababisha mmea kuonesha kwenye majani dalili za ugonjwa.
Kwa kuwa muhogo kwa kawaida huzalishwa kwa njia ya vipandikizi ugonjwa huu huingizwa kwenye sehemu mpya zilizopandwa kwa kutumia vipandikizi vilivyoambukizwa.
Kwa aina zinazovumilia sana kwenye hali za mabondeni, dalili mbaya sana hutokea wakati ugonjwa ukigundulika katika hatua za mwanzo.

Uchunguzi umeonesha kwamba Bemisia afer ni mdudu/kisababishi ambacho ndicho kinachohusiana na maendeleo ya hivi karibuni kuhusu uhamishaji wa visababishi kama “ipomovirus”. Mara nyingine inaonesha nzi weupe (White flies) na kutokana na hali hiyo bado uchunguzi unaendelea zaidi.

Udhibiti/Kuzuia
Njia ya msingi ya kuzuia/kudhibiti ugonjwa wa CBSD ni kuchagua mbegu kutoka kwenye mimea isiyo na dalili ya ugonjwa.

Ubora wa mashina unahitaji kutunzwa kwa kuendelea kuchagua na kuangamiza ile iliyoambukizwa ambayo inaonekana wakati wa kuchipua.

Hakikisha kuwa unapanda mbegu bora za mhogo ambazo zinastahimili uambukizo wa magonjwa.

Hakikisha kuwa wakati wa uvunaji uonapo hali ya kuoza kwa mizizi ya mhogo ichome moto ili kutokomeza ugonjwa huo.

Kuelewa dalili za ugonjwa wa CBSD kwa ajili ya kuchukua tahadhari ya kutokomeza ugonjwa huu.

Hakikisha kuwa unaendelea kutunza mbegu bora zinazoonekana kuvumilia magonjwa sana.

Hakikisha kuwa shamba la mhogo linakuwa safi kwa ajili ya kupunguza visababishi vya ugonjwa wa CBSD

b) Ugonjwa wa batobato au ukoma wa majani
Ni ugonjwa ambao ulienezwa kwamara ya kwanza hapa Tanzani mwaka 1894, na baadae uliripotiwa katika nchi nyingine nyingi za Afrika Mashriki, Afrika Magharibi na Afrika ya Kati na sasa unafahamika kuwa upo maeneo yote yanayolimwa muhogo Afrika.

Katika viwango vya kuwepo kwa ugonjwa wa CMD na katika uwingi wa hasara zinazopatikana kutokana na CMD ni kati ya 15% – 20%. Hii ni sawa na tani milioni 15 – 18 zikilinganishwa na makadirio ya shirika la kilimo na chakula duniani ya tani milioni 85 ya mwaka 1997.

Visababishi
Tangu ugonjwa wa CMD ulipoenezwa kwa mara ya kwanza, visababishi vilichukuliwa kuwa ni virusi kwa sababu ya kukosekana kisababishi kingine. Kwa hiyo kutokana na kuwa mtazamo huu unalingana na matokeo ya uchunguzi wa awali inaonesha kwamba ugonjwa huu huenezwa na nzi mweupe (white fly).

Pia uchunguzi wa mara kwa mara umesababisha utambuzi wa virusi vya aina mbalimbali na tofauti kama ifuatavyo:

• Ugonjwa wa batobato unaosababishwa na virusi vya Africa cassava mosaic virus

• Ugonjwa wa batobato unaosababishwa na virusi vya Afrika mashariki (East Africa cassava mosaic virus)

• Ugonjwa wa batobato unaosababishwa na virusi vya India (Indian cassava mosaic virus)

Dalili za ugonjwa wa batobato (Cassava Mosaic Disease-CMD)

Dalili hutokea kwenye jani lenye uwaraza wa michirizi ambazo huathiri

Sehemu zisizokunjamana za kutolea hewa na hufahamika katika hatua za

Awali za ukuaji wa jani.
Sehemu za kloritiki hushindwa kutanuka hadi mwisho, hivyo mvutano unajitokeza kutokana na ukuaji usiolingana na jani au majani madogo yaliyoharibika.

Majani yaliyoathirika sana hupungua ukubwa wa umbo, na hujikunja na kujitenga kwa sehemu zenye rangi ya njano na zenye rangi ya kawaida ya kijani.

Mmea hudumaa na majani machanga hupatwa na uvimbe.
Kloritiki ya jani inaweza kuwa ya rangi ya manjano nyepesi au rangi inayokaribia nyeupe yenye kijani kidogo au kupauka kuliko ilivyo kawaida.

Uambukizaji na uenezaji
Ukoma wa mhogo huambukizwa kwenye vipandikizi vya shina ambavyo kwa kawaida hutumika kuzalishia mmea.
Pia huenezwa na inzi mweupe (white fly) aitwae Bemisia tabaci G. Aina mbili za inzi au Mbu hao Bemisia (Preisner Hhosny na Aleorodius disperses R) pia huambukiza mihogo katika nchi za Afrika na India Usambazaji wa vipandikizi unaweza kusababisha kuenea kwa ugonjwa CDM katika Maeneo mapya.

UHIBITI NA KUZUIA
-Hatua ya msingi ya kuzuia ugonjwa wa CMD ni kwa kuchagua vipandikizi kutoka kwa Mmea ambao hauna uambukizo wowote.

-Ubora wa mashina unahitajika kwa kuendelea kuchagua na kuangamiza kwa kung’oa ile Mihogo iliyoambukizwa ambayo inaonekana wakati wa kuchipua

-Hakikisha kuwa wakati wa kuvuna mihogo kwa ile iliyoathirika na ugonjwa wa CMD inaangamizwa kwa kuchomwa moto.

-Hakikisha kuwa unatunza shamba na kuwa safi ili kupunguza wadudu waenezao CMD.

-Hakikisha una elimu ya kutosha juu ya dalili za ugonjwa wa CMD>

WADUDU NA WANYAMA WAHARIBIFU
- Cassava Mealy Bug (CMB)

Wadudu hawa hushambulia kwenye ncha za mashina/matawi kwenye majani machanga. Athari zake ni kwamba majani ynadumaa na kujikusanya pamoja, hivyo basi kupunguza ukuaji wa mmea kwa ujumla. Vile vile urefu kati ya pingili na pingili huwa fupi sana.

- Cassava Green Mites (CGM)

Wadudu hawa hushambulia majani mapya sehemu za chini. Madhara yake sio makubwa.

- White Scales
Hawa ni weupe na hujishika kwenye shina na kufyonza maji kutoka kwenye mti wa muhogo. Vili vile wadudu hawa madhara yake sio muhimu.

- Mchwa
Hawa hutafuna/hula mashina ya muhogo hasa wakati wa jua kali/kiangazi.
- Wanyama waharibifu
Hawa hushambulia muhogo ukiwa shambani kwa kuula, kama vile nguruwe, panya, wezi, n.k

Udhibiti/Kuzuia
Kwa upande wa wadudu wanweza kudhibitiwa kwa njia zifuatazo:

Kutumia dawa za kuulia wadudu

Kutumia wadudu marafiki wa wakulima

Kwa upande wa wanyama ni kuweka walinzi.Tupigie kupitia namba 0718405318

NAMNA BORA YA KUSINDIKA NYANYA

https://scontent-lhr3-1.xx.fbcdn.net/v/t1.0-9/15094883_417356921986558_356636340443847665_n.jpg?_nc_eui2=v1%3AAeHq1bcpjJ19qpvN_G1LnFRfNtJYHUGfIxlpNFBaixvAwvO58LuBzFjmBQc_-lOWiXjothg4e4tz1SeBe3hXJQrIzTmjBk835Xh0DxdexTMp8mSDMRL8CRUXzNu7J5bjksQ&oh=5662250edc17a25cc8335156904fc4ef&oe=58E15143
Nyanya zinaweza kusindikwa kupata bidhaa mbali mbali ili kuepuka uharibifu wa zao, kuongeza ubora na thamani, na pia kuwezesha upatikanaji wake wakati wote.
Baadhi ya bidhaa zinazotokana na zao la nyanya ni kama vile nyanya za kukausha, Juisi, pesti au lahamu na sisi au urojo.


1. KUSINDIKA NYANYA KWA KUKAUSHA
Nyanya za kukausha zinatakiwa ziwe zimekomaa na kuiva vizuri. Aina ya nyanya zinazopendekezwa kukausha ni zile zenye Nyama nyingi kama vile Tengeru 97, Roma na Tanya.

VIFAA
Visu vikali visivyoshika Kitu, ungo, sufuria, Jiko, kaushio bora, mifuko ya plastiki na beseni.

MALIGHAFI
Nyanya zilizokomaa na kuiba vizuri na ngumu, Maji safi na Salama.

JINSI YA KUKAUSHA
Chukua nyanya zilizokomaa na kuiba vizuri kisha OSHA kwa Maji safi na Salama.
Kata nyanya katika vipande vyenye Unene wa wastani usiozidi milimita Tano kwani Unene ukizidi vipande havitakauka vizuri na Kupungua ubora.
Panga nyanya kwenye kaushio safi ili zikauke.
Wastani wa kilo moja ya nyanya unaweza Kutoa gramu 180 za nyanya zilizokaushwa.
Fingasha vipande Vya nyanya vilivyokaushwa kwenye mifuko safi isiyopitisha unyevu.
Weka Lebo na hakikisha lebo inaonesha muda wa kisha kwa matumizi kuwa Mwaka Mmoja kutoka Siku ya kutengenezwa.
Hifadhi kwenye sehemu yenye ubaridi na kavu.

MATUMIZI
Nyanya zilizokaushwa hutumika kama kiungo kwenye Vyakula mbali mbali.

2. KUSINDIKA NYANYA KUPATA JUISI
Nyanya kama matunda mengine huweza kusindikwa na kutengenezwa Juisi ambayo hutumiwa na watu wa rika zote.

VIFAA
Chupa zenye mifuniko imara, lebo, chujio au kitambaa safi, sufuria, ndoo au beseni, kisu kisichoshika Kitu, mizani na Mashine ya Kusaga nyanya.

MALIGHAFI
Nyanya zenye Juisi nyingi kama vile marglobe, money maker, Sukari nyeupe na chumvi.

JINSI YA KUTENGENEZA JUISI
Chagua nyanya zilizokomaa na kuiba vizuri kisha osha kwa Maji safi na Salama.
Katakata nyanya katika vipande kidogo kisha Pima uzito wa nyanya.
Kwa kilo moja ya nyanya, ongeza Maji kiasi cha Lita moja.
Chemsha kwenye moto wa kadiri (nyuzi moto 85 za sentigredi) kwa muda wa dakika 5.
Saga nyanya kwa kutumia Mashine ya mkono au Umeme kisha chuja rojo ili kupata Juisi.
Pima uzito wa Juisi na ongeza Sukari gramu 20 na chumvi gramu 10 kwa Kila Lita 1 ya Juisi.
Chemsha tena kwenye moto wa kadiri (moto la nyuzi 85 hadi 90 za sentigredi) kwa dakika 20.
Ipua Juisi na jaza Juisi Ikiwa ya moto kwenye chupa safi zilizochemshwa kisha zifunike na zipange kwenye sufuria.
Weka Maji ya uvuguvugu kwenye sufuria hiyo hadi yafike nusu ya kimo cha chupa kisha chemsha tena chupa hizo ili kuondoa hewa iliyopo Ndani ya chupa za Juisi na kuua vijidudu.
Ipua na acha zipoe, kisha weka lebo na lakiri.
Hifadhi kwenye sehemu yenye ubaridi safi na mwanga hafifu.
Juisi ya nyanya iliyotengenezwa kwa Njia hii huweza kuhifadhika kwa muda wa miezi Sita bila kuharibika.

MATUMIZI
Hutumika kama kiburudisho na hutupatia virutubisho vingi mwilini.
Virutubisho vinavyopatikana katika gramu 100 za Juisi ya nyanya ni kama ifuatavyo;
Maji. 94%
Wanga. 4.3g
Sukari. 3g
Madini ya Chuma 0.6g
Vitamini C. 61.7ml
Nguvu. 92 Kilokari
Vitamini A. 74 I.U

3. KUSINDIKA NYANYA KUPATA LAHAMU AU PESTI

VIFAA
Jiko, mizani, kisu kisichoshika Kitu, sufuria, chupa zenye mifuniko imara, lebo, Mashine ya Kusaga, meza ya Kukata na chujio.

MALIGHAFI
Nyanya zinazotoa rojo nyingi kama vile Roma na Tanya, wanga wa Mahindi, ndimu ya Unga, sodium benzoate na chumvi.

JINSI YA KUTENGENEZA
Chagua nyanya zilizokomaa na kuiva vizuri kisha osha kwa Maji safi na Salama.
Kata nyanya katika vipande kidogo kisha chemsha hadi ziwe lakini.
Chuja kupata Uji mzito na ondoa Maganda na mbegu.
Pima uzito wa pesti na weka chumvi gramu 40 kwenye kilo moja ya pesti.
Chemsha ukiwa unakoroga hadi pesti ibaki nusu.
Ongeza wanga utokanao na Mahindi kiasi cha gramu 20, ndimu ya Unga gramu 5 na mikrogramu 800 za sodium benzoate kwa kilo moja ya pesti.
Chemsha kwa muda wa dakika Tano na weka kwenye chupa Ikiwa bado ya moto.
Panga chu

pa zenye pesti kwenye sufuria na weka Maji kwenye sufuria hiyo hadi yafike nusu na kimo cha chupa.
Chemsha chupa hizo kwa muda wa dakika 20 ili kuondoa hewa na kuua vijidudu.
Ipua, acha zipoe kisha weka lebo na lakiri na kuhifadhi kwenye ubaridi.
Pesti iliyotengenezwa kwa Njia hii huweza kuhifadhiwa kwa muda wa miezi Sita bila kuharibika.

MATUMIZI
Pesti ya nyanya hutumika kama kiungo cha chakula na aina ya virutubisho vingi.
Virutubisho vinavyopatikana kwenye gramu 100 za pesti ya nyanya ni kama ifuatavyo;

Nguvu. Kilokari 442
Wanga. Gramu 19.6
Protini. Gramu 4.4
Maji. Gramu 75
Vitamini A. Miligramu 330
Vitamini C. Miligramu 17.8
Potasiamu. Miligramu 888
EPUKA UMASIKINI KILIMO NI PESA 0718405318 au 0767405318

FAHAMU KILIMO CHA UYOGA NA FAIDA ZAKE MWILINI UTANGULIZI.

https://scontent-lhr3-1.xx.fbcdn.net/v/t1.0-9/15284944_426041371118113_2726288047289448546_n.jpg?_nc_eui2=v1%3AAeHjjenP25Ryhg0M6PxBURAzXuoGsnqfQgdz9Cjiz6apXVVJ_pnRVO6Inc40CWnbvphuHS4ID4uoce-sXxBPZ5_Yp0dJj_XnmOLy26GXnyWibAXz-0ZcBYFXJtX8zmWeT6U&oh=f99ba5e047fd3af2213d751b9664ff9d&oe=58E0D531Uyoga ni aina ya nyuzi kuvu (fungus) yenye kutofautiana na mimea mingine kwa kukosa chembe chembe zinazowezesha mimea kujitengenezea chakula yenyewe kwa kutumia hewa na mwanga.
Uyoga unaota wenyewe kwenye mashamba hasa wakati wa mvua kwenye maeneo yenye mboji nyingi. Sasa hivi nchini tunao utaalamu wa kuotesha uyoga au ndani ya nyumba au nje kwenye kivuli maalumu.

HISTORIA FUPI YA UYOGA.
Uyoga umefahamika na wanadamu tangu enzi za zamani sana. Miaka elfu nne kabla ya kuzaliwa Kristo watu walijua uyoga. Historia inatueleza kwamba watu wameanza kulima kwa utaalamu mwaka 300 baada ya kuzaliwa Kristo.
Wadadisi wa mambo wanauelezea Uyoga kufanana sana na chakula waisraeli walichokuwa wakila kule jangwani katika safari yao ya kutoka utumwani Misri.
Wakati Uyoga ukilimwa katika dunia yote, hapa Afrika na hasa kwetu Tanzania mambo yalikuwa ni tofauti kabisa. Hakuna mtu aliyesumbuka na kilimo hicho. Ni hapo majuzi tu mwaka 1993 ndipo ukulima ulianza Dar es salaam. Mwaka 1994 ukulima ulianza Arusha, mwaka 1995 ukulima ulianza huko Mbeya, na mwaka 2003 ukulima ulianza huko Kilimanjaro.

AINA YA UYOGA.
Inakadiriwa kuwa kuna aina milioni moja na laki tano (1,500,000) za nyuzi kuvu (fungus) duniani; katika hizi ni aina 64,000 ambazo zimekwisha kufanyiwa utafiti na kupatiwa maelezo ya kisayansi. Katika hizi aina 64,000, kuna ambazo zimethibitika kuwa na Uyoga halali 12,000. Na kati ya hizi ni aina 2,000 na ndizo zinazolimwa.
Katika aina 2,000 za uyoga zilizokwisha thtbitika, hapa Tanzania ni aina 40 tu.
Uyoga Mamama (Oyster mushroom).
Aina hii ya Uyoga hustawi katika nchi za Tropics. Utaalamu unaohitajika siyo mgumu. Baadhi ya aina zinazooteshwa ni hizi zifuatazo;
. Pleurotus oystreotus
. Pleaurotus sajo-caju
. Pleaurotus sapidus
. Pleurotus flabel atus - (pink oyster)
. Leaurotus Pulmonerius
. H. K. n.k
. Monkey Head
. Auriclaria
Nyingine zinazooteshwa hapa nchini kwa kiasi kidogo ni;
. Agaricus bitoquis (uyoga vifungu)
Uyoga taka ambazo ni;
. Coprinus cinereus
. Caprinus Comatus
. Lentinus edodes
. Volvoriella Volvocea
Nyingine ni;
. Ganodema lucidum

FAIDA ZA UYOGA
Uyoga una maajabu makubwa katika maisha ya mwanadamu, Uyoga ni lishe bora kwa mwanadamu, ni dawa na tiba kwa mwanadamu, ni zao la kuingizia watu kipato, ni rafiki wa mazingira pia.
LISHE
. Uyoga ni zao lenye viini lishe (amino acids) zote 22 zinazohitajika na mwili wa mwanadamu.
. Protini iliyoko kwenye Uyoga inafikia kiwango cha asilimia arobaini. Hii inalingana na protini iliyoko kwenye maziwa.
. Kuna wingi mkubwa sana wa vitamini B,C na D.
. Uyoga hauna mafuta mengi. Una asilimia tatu tu. Hivyo hauna Colestrol.
. Uyoga unayo madini yote muhimu kwa mwanadamu; phosphorus, Iron, Calcium na Potash.
TIBA
Utafiti uliofanyika siku za karibuni umethibitisha kuwepo kwa dawa nyingi ndani ya uyoga zenye uwezo wa kutibu kwa ufanisi, magonjwa ya wanadamu na mifugo. Kwa wanadamu magonjwa yafuatayo yanatibiwa;
. Kifua kikuu TB
. HIV/AID upungufu wa kinga mwilini
. Kisukari
. Shinikizo la damu
. Magonjwa ya moyo na uti wa mgongo
. Saratani
. Matatizo ya figo
. Vifo vya watoto wachanga
AJIRA
Kwa sasa hivi ajira imepungua sana katika nchi yetu. Vijana, wazee na rika lote hatuna kazi, mazao yaliyokuwa yakituingizia kipato yamepungua au yamekwisha. Nguvu kazi nyingi tuliyonayo inatumika kuuza mwanasesere na plastic zinazotoka katika nchi za nje.
Watu wengi mno tunaishi katika lindi la ufukara. Hatuna mahitaji ya msingi kama vile chakula, malazi na mavazi bora. Kufuatana na ripoti ya umoja wa mataifa, iliyoandaliwa na Professors S. T. Chang na Mshigeni wa chuo kikuu cha Namibia, mauzo ya Kahawa kwenye soko la ulimwengu kwa mwaka 1997 ni dola za kimarekani bilioni 15. Mauzo ya Uyoga yalikuwa dola bilioni 14. Katika biashara hiyo Afrika ilichangia kwa asilimia 0.3 tu.
Wataalamu hawa wanaainisha sababu nyingi zinazosababisha upungufu huu. Kubwa wanalosema ni kuwa waafrika hawajui umihimu wa uyoga katika maisha ya mwanadamu. Bei ya uyoga huko Marekani, Mashariki ya kati na Mashariki ya Mbali ni kati ya dola za Marekani tisa ($9) hadi kumi na tatu ($13). Uyoga ni zao lililo kayika mpango nafuu wa biashara ya Marekani na Afrika. Halitozwi ushuru kuingia katika masoko ya Marekani.

KUSAFISHA MAZINGIRA
Kufuatana na ripoti ya wataalamu wa chuo kikuu Kivais na Magingo ya miaka ya tisini, Tanzania inayo masalio ya kilimo na misitu zaidi ya tani milioni kumi na saba (17,000,000). Masalio haya yameachwa yakioza, au kuchomwa moto au kulishwa mchwa pamoja na mapanya. Ikiwa masalio haya yatatumika kuoteshea Uyoga, Mazingira yataboreka na uchumi utakua. Uzalishaji wa Uyoga unaanzia pale mkulima au mtumiaji wa bidhaa za kilimo na misitu anapomalizia.

MASALIO YA TAKATAKA BAADA YA KUOTESHA UYOGA.
Masalio ya takataka (vimeng'enywe) hutumika kama ifuatavyo;
. KULISHA MIFUGO
Uyoga una uwezo wa kuvunja vunja chembe chembe za vimeng'enywe na kuviboresha kuwa protini na madini mengi, kisha kufyonza hicho na kutengeneza matunda ya uyoga. Baada ya kuvuna uyoga chembechembe hizi bado zina ubora mkubwa wa chakula kwa ajili ya mifugo kama vile ng'ombe, mbuzi, nguruwe, sungura n.k. Tunao wafugaji wanaotumia vimeng'enywe hivi kulishia mifugo nao wameendelea kupata maziwa mengi.
. MBOLEA
Vimeng'enywe hivi hutumika kama mbolea shambani na katika bustani. Matokeo ya kutumia vimeng'enywe hivi yameonyesha ufanisi mkubwa.
.METHANE GAS
Tukijenga mfumo wa kutengeneza gesi kama kawaida, tunaweza kutumia vimeng'enywe hivi kutengeneza methane gas. Hii gesi itatumika kupikia, kuwasha taa na mambo mengine kama hayo. Mabaki katika zoezi hili huwa na mbolea nzuri ifaayo sana. Mazao ya shamba na bustani yaliyokuzwa kwa mbolea hii yana bei nzuri zaidi sokoni, maana yanahesabika yamezalishwa kiasili (organic agriculture).
. ZERI ( Zero Emmission Research Initiative).
Umoja wa Mataiga umeiteua Tanzania pamoja na nchi nyingine katika bara la Afrika kuendeleza na kutekeleza mfumo wa ZERI. Huu ni mfumo wa kutochafua mazingira kwa njia ya kutoa moshi. Masalia ya kilimo ba misitu yasichomwe moto bali yageuzwe kutoka hali yake na kuwa kitu kingine labda kilicho bora na chenye thamani zaidi. Masalia ya sokoni hatutayaacha yaoze bure, tutayasindika ili yaweze kuzalishia uyoga. Pumba za mpunga na kahawa hatutazichoma moto. Tutazitumia kwa kuzitengenezea chipboards, vivyo hivyo na maranda ya mbao, takataka za katani, kahawa na n.k. zitageuzwa kuwa kitu bora zaidi.

UTAYARISHAJI WA SHAMBA LA UYOGA.
Mambo ya muhimu ya kuzingatia:
. Ukubwa wa shamba
. Uwezekano wa upanuzi
. Usafi wa eneo
. Upatikanaji wa takataka za kulimia yaani vimeng'enywe
. Upatikanaji wa maji safi
. Umbali kutoka kwenye soko
Ndani ya ndani
. Hewa safi ya inayozunguka
. Joto linalotakiwa
. Unyevunyevu kwenye hewa unaotakiwa
. Carbondioxide na mwanga vinatakiwa
Shamba
Shamba la uyoga linapaswa liwe na viambatanisho vifuatavyo;
. Sehemu ya kutayarisha vimeng'enywe
. Kichanja cha kuhifadhi majani au aina yoyote nyingine ya vimeng'enywe.
. Sehemu ya kuchemshia vimeng'enywe
. Sehemu ya kupandia mbegu kwenye vimeng'enywe vilivyokwisha kuchemshwa.
. Banda kamili la kukuzia lenye sifa zilizokwisha ainishwa hapo juu
. Sehemu ya kuhifadhia uyoga uliovunwa au chumba cha baridi kutegemea na hali halisi.

UJENZI WA SHAMBA
Mkulima anashauriwa kutumia vifaa vinavyopatikana katika eneo lenyewe. Kwa mfano mkulima mwenye shamba la migomba, baai atumie marawa katika kuta na paa. Unaweza ukatumia nyasi za kawaida au majani ya mpunga, ngano na mengine ya namna hiyo, unaweza kutumia matofali mabichi, unaweza kutumia mabanzi. Ndani ya nyumba weka weupe. Hii ni chokaa au kitambaa cheupe. Hii ni kwa sababu uyoga hukua kuelekea rangi ya mazingira yaliyouzunguka. Lakini rangi nyeupe huchochea ukuaji na hudumisha usafi. Nyumba ya uyoga iwe na madirisha makubwa mazuri.

MAANDALIZI YA VIMENG'ENYWE
Kama ilivyosemwa hapo mwanzo, kila jani lililokomaa na kukauka, lafaa kuoteshea uyoga. Michanganyiko ifuatayo yafaa sana kuoteshea uyoga.
. Majani ya mpunga au migomba yenye unyevu 62%
. Pumba za mahindi unyevu 62%
. Sukari
. Chokaa
Vimeng'enywe viko vingi, mkulima anashauriwa awaone wataalamu kwa ushauri.
MAHITAJI MENGINE
Ifuatayo ni orodha ya mahitaji mengine;
. Jiko la kuchemshia
. Pipa tupu la lita mia mbili
. Mifuko ya plastic size 10" × 15" yenye uwezo wa kuhimili joto
. Viroba (polysacks) pvs ya kuweka ndani ya pipa
. Vibangili vya kipenyo cha 1.5
. Kamba au uzi wa kushonea viatu ili kufunga mifuko wakati wa kuchemsha.
. Vipande vya magazeti
. Rubber band size ya mpira wa ndana ya tairi ya baiskeli.

HATUA ZA KUFUATA KATIKA KUOTESHA
. Katakata majani yaliyokomaa na makavu katika urefu usiozidi nchi nne
. Changanya majani haya na virutubisho hapo juu i.e. pumba za mahindi, sukari na chokaa.
. Changanya sawasawa kwa kutumia maji safi ndoo tatu hadi tano.
. Zilundike mahali safi ukitengeneza mlinduko wenye kimo cha mita moja hadi mita moja na nusu.
. Funika kwa polythene paper na vitambaa vya sulphate
. Majani ya migomba yalowekwe kwa siku mbili hadi tatu kabla ya kuvundikwa
. Ziache kwa muda wa masaa 24
. Weka vimeng'enywe hivi katika mifuko ya polythene
. Weka maji lita 40 katika pipa lenye kichanja cha mbao chenye kuzuia mifuko isigusane na maji
. Bandika kwenye jiko hadi mvuke unapotoka , hesabu msaa manne.
. Ipua mifuko yako na iweke mahali safi
. Sasa ni wakati wa kufanya kila kitu kwa hali usafi. Tunatumia maji yenye detol kusuzia mikono yetu
. Otesha uyoga kama mtaalamu atakavyokuonyesha
. Baada ya siku 21 ondoa vipande vya gazeti ulivyotumia kufunika mifuko
. Baada ya siku 10 nyingine utaanza kuvuna uyoga. Uta una kwa muda wa miezi 2 hadi 3
. Weka uyoga uliovuna ili kuhifadhi ubora wa uyoga.
MAPATO YA MKULIMA
Tunaorodhesha hapa hali halisi ya mkulima wetu mwenye banda la mita tatu (3) kwa mita tano (5).
Gharama:
Majani ya mpunga Pickup moja = 25,000/-
Mifuko ya plastic 500@50 = 25,000/-
Mbegu za uyoga chupa 100@1500 = 150,000/-
Jumla = 200,000/-

Mavuno aliyopata kilo 300@3000 = 900,000/-
Toa gharama = 200,000/-
Salio = 700,000/-
Kazi hii ilimchukua mkulima huyu miezi mitatu. Ijulikane kuwa baada ya kuotesha mkulima anakagua banda kw muda mfupi sana, asubuhi saa sita na jioni. Mkulima huyu na familia yake anajipatia wastani wa shilingi 230,000/- kila mwezi kwa kulima banda moja.
MAPISHI
Mkulima na umma wote wanapashwa kujua mapishi ya uyoga.
Tunaweza kutumia uyoga kama ifuatavyo;
. Kutengeneza supu
. Kutengeneza supu ya viungo (mushroom curry)
. Kutengeneza mboga ya kawaida tunayoweza kula na vyakula vingine kama vile ugali ndizi, wali, viazi n.k.
. Tunaweza kuzindika a kutengeneza mushroom pickle (hii tutauza kwenye supermarket na mahoteli ya kawaida hasa ya kitalii)
. Tunaweza kutengeneza mushroom pizza.

MAGONJWA YA UYOGA
Uyoga ni viumbe hai. Hivyo hupatwa na magonjwa kama hali ya mazingira na utendaji haitakidhi. Kuna magonjwa ya aina kama ifutavyo;
. Bacteria
Uyoga unakuwa na rangi ya kutu. Hata mifuniko inakuwa na rangi hiyo. Ugonjwa huu unatambulika kiurahisi., kwani unakuwa unateleza.
. Fungus
Aina zifuatazo ndizo hasa zishajulikana;
. Blue mould
. Black mould
. Brown mould
. Virus
Uyoga uliopendeza unasinyaa mara moja. Unaanza kutoka jasho.

MASOKO
Mpaka sasa hoteli za kitalii zinapika uyoga wa kutoka nje uliowekwa kwenye makopo.
Ikumbukwe kuwa kwenye makopo kuna uyoga halisi kidogo sana. Pia katika supermarket za hapa nchini kuna uyoga fresh kutoka Kenya. Pia tujue kuwa majirani wetu waliotuzunguka Kenya, Uganda, Zambia na Malawi wamepiga hatua kubwa katika kilimo cha uyoga. Swali tunalopaswa tujiulize sote ni hili " Kulikoni Tanzania kuhusu Uyoga".
Tumeziona faida za uyoga. Ni bora kuliko nyama nyekundu na nyama nyeupe. Kwenye maduka ya nyama zinauzwa kilo nyingi za nyama kila siku. Badala yake tuuze uyoga kila siku.

SOKO LA NJE
Kama ilivyoelekezwa hapo juu kuna masoko ya nje. Lakini yanataka kiasi kikubwa cha uyoga. Tani kadhaa kila wiki na kila mwezi. Ili kuweza kukidhi haja hii, wakulima waunde vikundi na vyama vya ushirika ili kushughurikia jambo hili.. EPUKA UMASIKINI KILIMO NI PESA.WASILIANA NASI KUPITIA 0718405318 AU 0767405318

JIFUNZE UFUGAJI BORA WA NYUKI



Ufugaji wa nyuki unaweza kuwa chanzo kizuri cha kipato cha ziada kwa wakulima wadogo wadogo.

Uzalishaji wa asali nchini Tanzania umekuwa ukitegemea sana wafugaji wadogo wadogo, wanaotumia njia za kiasili kama vile mizinga ya magogo au vyungu, kwa nyuki wa kiafrika ambao ni wengi sana kwenye mapori.

Ni muhimu kuwa na utaalamu wa kufuga nyuki
https://scontent-lhr3-1.xx.fbcdn.net/v/t1.0-9/15327460_424697091252541_6524844317101705452_n.jpg?_nc_eui2=v1%3AAeEf1trFjsPp84hznEl3hbCnJssjjCVCjE03-XwsXnn-B5dpwxeiIfK1dwhk9VNz5L16n25yKsEvTJUL3HdYh89ZAcO78bR-LgIuegSG-jrtKg7iRIXplA41YgL-16m_G_g&oh=d181f89d81390424091ac1d122073de7&oe=58DAD248
Mkulima ambae anahitaji kufuga nyuki ni lazima awe na uelewa wa mzunguko wa maisha ya nyuki. Anaye anza ni lazima aulize wafugaji wenzake ambao wana uzoefu wa kutosha, au kujiunga katika kikundi cha ufugaji ili apate ufahamu zaidi juu ya ufugaji wa nyuki.

Tafuta sehemu salama kwa ajili ya mzinga

Ni vizuri kutafuta mahali pazuri, salama, na penye sifa ya kufugia nyuki. Vifaa vyote vikishapatikana jambo linalofuata ni kuchagua mahali gani pa kuweka mzinga. Ni vizuri sehemu hii ikawa mahali ambapo makundi ya nyuki hukusanyika mara kwa mara.

Ni wapi pa kuweka mzinga!

Mara nyingine kupata eneo sahihi ni tatizo. Ni vizuri kuzingatia yafuatayo:

• Kulingana na hali ya kujilinda ya nyuki wa Afrika, haishauriwi kuweka mzinga shambani au karibu na shamba (weka umbali wa mita 150-200 kutoka kwenye mazao au nyumbani)
• Mzinga ni lazima uwekwe sehemu ambayo haitasababisha upotevu wa nyuki wanaporudi kutoka nje ya mzinga (wasiingie kwenye kundi lisilokuwa lao)
• Mizinga isiwekwe mbalimbali sana ili kuepusha usumbufu wa kutembea mbali kwa mfugaji wakati anapokagua. Eneo la kuweka mizinga ni lazima liwe :
• Kimya na mbali ya jumuia (hospitali, shule, na viwanja vya michezo) na maeneo ya biashara au viwanda.
• Karibu na maji masafi-kandokando ya mto, mabwawa ya samaki, mabeseni ya maji au sehemu ya matone.
• Iwe karibu na chakula cha nyukimimea inayochanua, miparachichi,
nazi, euculptus, migunga n.k
• Iwe sehemu ambayo ni kavu na isiwe sehemu ya tindiga kwani unyevu unyevu husababisha ugonjwa wa ukungu (fungal disease) na pia huzuia utengenezaji mzuri wa asali.
• Iwe mbali na watu waharibifu na iliyojificha kuepuka waharibifu.
• Sehemu ya mizinga ni lazima iwe inafikika kirahisi kwa kipindi chote cha mwaka ili iwe rahisi kuhamisha nyuki pale inapohitajika.
• Kuwe na kivuli cha kutosha hasa wakati wa mchana jua linapokuwa kali, na kusiwe na upepo mkali.
• Iwe mbali na mashamba, ambapo dawa za kuulia wadudu zinatumika.
Vichaka au wigo unaotenganisha mizinga na kuzuia wavamizi ni muhimu ili kupunguza ukali wa nyuki.

Jinsi ya kuweka mzinga

Baada ya sehemu ya kuweka mizinga kupatikana, kinachofuata ni kuandaa mizinga kwa ajili ya kuweka panapotakiwa.
• Safisha mzinga kuondoa uchafu wote, utando wa buibui na aina nyingine za wadudu.
• Weka chambo kwenye mzinga (waf ugaji wa nyuki mara nyingi hutumia nta) kwa kuipaka katika kuta za mzinga kwa ndani.
• Mzi nga unaweza kutundikwa kwenye mti, kwenye nguzo, kuweka kwenye jukwaa au kwenye miamba. Hii inategemea mkulima mwenyewe anapendelea njia ipi.

Aina za mizinga ya nyuki

Kifuniko juu (Top bar)

Hii ni aina ya mizinga inayotumika sana. Gharama yake ni karibi shilingi elfu hamsini za kitanzania. Ni aina nzuri sana kwa mtu anaeanza ufugaji wa nyuki kwa kuwa ni wa gharama nafuu. Hata hivyo mfugaji wa nyuki anaweza kutengeneza mzinga mwenyewe kama ana utaalamu wa useremala.

Faida

• Ni rahisi kukagua asali iliyo tayari.
• Ni rahisi kuvuna asali kuliko kuvuna toka kwenye mzinga wa kienyeji.
• Ni rahisi kuwatunza nyuki wakati wa kiangazi na inapokuwa hakuna maua. Mfugaji anaweza kuwapatia nyuki chakula ili kuongeza uzalishaji wa asali.
• Kurina asali ni rahisi sana ukilinganisha na mizinga ya magogo inayotundikwa juu ya mti, kwa kuwa haihitaji vifaa maalumu.
• Aina hii ya mizinga huwekwa kwa kuninginia jambo ambalo siyo rahisi kushambuliwa na wadudu/wanyama wanaokula asali. Inajaa haraka sana wakati ambao ni msimu wa asali kutengenezwa kwa wingi.

Hasara

• Kichane kwenye mzinga wa boksi hakina kishikizo hivyo huvunjika kwa urahisi sana kama hakitashikwa kwa uangalifu.
• Masega huvunwa pamoja na asali, jambo linalolazimu nyuki kutengeneza tena masega mengine na husababisha kupungua kwa uzalishaji wa asali.

Mzinga wa Langstroth unaweza kukupatia asali zaidi

Hii ni aina nzuri na rahisa sana ya mzinga. Pia hufahamika kama mzinga wa fremu, kwa kuwa ina fremu ambazo vichane vya masega hujishikiza. Pia una chumba kikubwa ambacho malkia hutagia mayai. Malkia anazuiliwa kuhama kwenda chumba kingine kwa kutumia waya. Kwenye chemba maalumu ya kutagia juu yake pana chemba ya kuhifadhia asali. Vichane vya masega vinatengezwa kwenye fremu na si kwenye nguzo kama ilivyo kwenye Top bar.
Ili kuvuna asali, mfugaji akiwa na masega yaliyojaa asali, hutumia vifaa maalum kwa ajili ya urinaji na kuhifadhi asali bila kupata tabu.
EPUKA UMASIKINI KILIMO NI PESA.wasiliana na Kilimo Na Mkulima Tanzania kupitia 0718405318 au 0767405318.

FAHAMU MAMBO MUHIMU YA KUZINGATIA KABLA HUJAINGIA KATIKA KILIMO CHA BIASHARA.

Kabla haujaamua kuingia katika kilimo cha biashara inakupasa kwanza ufahamu mambo muhimu ambayo yatakusaidia katika shughuri yako ya kilimo husika.Kwani yakupasa kutambua kila kazi ya kuingiza kipato ina changamoto zake na kilimo ni moja ya kazi yenye changamoto nyingi ambazo yakupasa nyigine ujipange jinsi ya kukabiliana nazo kabla ya kuaingia katika kilimo husika.
Mambo hayo muhimu ni
https://scontent-lhr3-1.xx.fbcdn.net/v/t1.0-9/15589485_435477463507837_2393623494652658756_n.jpg?_nc_eui2=v1%3AAeFiqJH6z1PMfQ0kf8FeUW5XX_Q0C2x0uONTj89jeqT2E3_1KzAW853uhWIJoYb4nYn4jEVlL2tqIyoDzWnSF2YgtL6odwSBR9ij67YoC-_dxwYVkzpLFvT3xUXhXGX4uMI&oh=9ed32f8c57961d99f9af4cd1081ce803&oe=58DC7DB7
1>UTAYARI KUINGIA KATIKA KILIMO
Inakupasa kabla hujajiingiza katika kilimo uwe tayari wewe mwenyewe kuamua kuanza kufanya kufanya kilimo husika,Kwa maana nyingine namaanisha maamuzi yako ya kuingia katika kilimo yatokane na uchaguzi wako mwenyewe baada ya kuangaliaya na kuona kilimo ni moja ya jambo litakaroboresha kipato chako.Ili kuepuka kujiuliza uliza maswali ya uamuzi wako wa kwanini na nani amekushauri kuingia kufanya shughuri hiyo ya kilimo husika,Hivyo utayari wako utakusaidia kuongeza ari na juhudi zaidi katika kazi yako na kukupunguzia kukata tamaa njiani.

2>UCHAGUZI WA KILIMO KINACHOKUFAA
Kabla ya kuingia katika kilimo lazima kwanza ufanye uchaguzi wa kilimo gani ambacho utafanya.Katika Uchaguzi lazima uchague kitu ambacho utakuwa tayari kukifanya bila kupata pingamizi la utayari wa kufanya kilimo hicho.Katika uchaguzi unaweza kuchagua kilimo mchanganisho kwa maana kulima mazao na kufuga mifugo au kulima mazao/kufuga mifugo tuu.
Na hapa katika uchaguzi ukichagua kilimo ambacho si sahihi kwako ndipo ambapo husababisha changamoto nyingi katika kilimo chako hapo baadaye.Hivyo uwe makini katika kuchagua Mazao/Zao,Mifugo/Mfugo sahihi kwako kutokana na utakavyojiangalia utayari wako.Pia suala la uhakika wa uwepo wa soko la utakachochagua kukifanya ni kitu cha msingi katika kilimo chako,Kwani yakupasa utambue hapo baadaye utahitajika uuze ulichozalisha hivyo usipokuwa makini inaweza kusababisha hasara kubwa katika kilimo chako.Na yakupasa kutambua kuwa bei hubadilika badilika kulingana na msimu wa mavuno na bei za soko.

3>UTAFITI NA USHAURI WA GHARAMA JUU YA KILIMO ULICHOKICHAGUA
Baada ya kufanya uchaguzi wako inakupasa ufanye utafiti wa gharama utakazoweza kuzimudu katika kilimo chako.Hili litaendana na Ushauri wa Jinsi gani ya kuweza kufanya kilimo chako kwa gharama nafuu zaidi ili kama ikitokea hasara uwe na uwezo wa kuikabili vizuri.

4>PANGA BAJETI YAKO KABLA HUJAANZA KILIMO
Yakupasa upange bajeti yako kabla hujaanza kilimo kwa kuangalia utafiti na ushauri wa gharama juu ya Kilimo ulichokichagua.Hi itakusaidia katika manunuzi na malipo ya huduma muhimu katika shughuri zako kwani utakuwa umejipanga mapema kukabiliana na matatizo yatakayohitaji fedha ya mfukoni kwa ajili ya huduma kama madawa,mbegu n.k
Kumbuka* malipo ya watakaohudumia kilimo chako usiyasahau katika bajeti yako na yataendana kulingana na idadi ya utakaowaajiri.

5>USIMAMIZI MZURI
Baada ya Kupanaga mipango yako usisaha katika kupanga vizuri usimamizi wa kilimo chako na hapa ukifanya makosa kamwe hutoweza kufanikiwa na kuishia kukiona kilimo hakifai hata kama ulitoa gharama zote zilizohitajika wenyewe wanasema uchungu wa mwana ajuaye mzazi,,wakulima tunasema uchungu wa kilimo aujuaye mkulima,Msemo huu,hii ianamaanisha uangalizi wako kwa ukaribu katika kilimo chako unahitajika zaidi kuliko kuwa mtu wa kuagiza tuu bila kufuatilia maendeleo ya kilimo chako wakati kinafanyika.

6> TAFUTA USHAURI WA UTAALAM WA KILIMO ULICHOKICHAGUA
Kabla hujaanza usisite kutafuta ushauri wa kitaalam wa kilimo ulichokichagua.Ili uwe karibu na kugundua tatizo katika kilimo chako kabla hujachelewa sana kupata athari ya tatizo husika.Na pia hili litakusaidia kufanya kilimo chako kwa uhakika zaidi.

7> ANZA KILIMO CHAKO KWA UHAKIKA
Mwisho baada ya kupitia hatua hizo juu anza kufanya kilimo chako kwa uhakika zaidi na Pia huku unatambua kilimo nacho ni biashara kama zilivyo biashara nyingine hivyo uwe makini katika kilimo chako ili kujiepusha na changamoto zitakazojitokeza katika kilimo chako na changamoto hizo zisiwe kikwazo katika kukuzuia kuendendelea na kilimo chako.. EPUKA UMASIKINI KILIMO NI PESA.WASILIANA NASI KUPITIA NAMBA 0718 405318 AU 0767405318